
Msanii wa nyimbo za injili nchini, Rose Mhando, ameshtakiwa kwa Waziri
wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, kwa kitendo cha
utapeli na kushindwa kutekeleza mkataba wa kuhudhuria na kutumbuiza
kwenye Tamasha la Pasaka lililofanyika jijini Mwanza licha ya kulipwa
gharama zote alizotaka.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions inayoongozwa na Alex Msama,
ambayo ina mkataba naye imekuwa ikiuza na kuandaa matamasha ya msanii
huyo pamoja na tamasha la Pasaka la kila mwaka, alimweleza Waziri
Nnauye, mbele ya halaiki ya wananchi alipokuwa mgeni rasmi wa sherehe za
tamasha hilo lililofanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza na mikoa ya
Kanda ya Ziwa.
Msama alieleza kusikitishwa na kitendo cha Rose Mhando kuingia mitini
ilihali akiwa ameingia mkataba na kulipwa gharama zote pamoja na nauli
alizodai kabla ya kuanza safari kufika Geita, Mwanza na Kahama kujiunga
na wasanii wenzake kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha hilo.
“Mheshimiwa Waziri, Rose Mhando naye amekuwa ni jipu kwa kuwa amefanya
utapeli kwa kukubali kulipwa gharama zake zote lakini ameshindwa
kuhudhuria na kutumbuiza kama wenzake wakina Solomon Mkubwa, Bonny
Mwaitege, Upendo Nkone na wengine uliowashuhudia hapa.
“Hii ni mara ya tatu amekuwa akifanya hivi na mara kwa mara nimekuwa
nikimsamehe,” alisema bila kutaja kiasi alichomlipa katika mkataba
waliokubaliana ili aweze kufanya onyesho hilo.
Msama pia akatumia fursa hiyo kuwaomba radhi wananchi waliofika katika
Uwanja wa CCM Kirumba kwa kutegemea mwimbaji huyo angekuwepo na
kutumbuiza na wenzake lakini kilichotokea ni aibu na utapeli wa msanii
huyo mkubwa wa nyimbo za injili aliyejizolea umaarufu ndani na nje ya
nchi.
“Kuanzia leo mtu yeyote asije akaingizwa mjini na Rose Mhando kwa
kuingia naye makubaliano akidhani yupo chini ya Kampuni ya Msama
Promotions, kwa kitendo alichoendelea kukifanya naomba kutangaza rasmi
kuvunja mkataba wa kufanya kazi na msanii huyo ili kulinda hadhi na
heshima ya Kampuni yangu,” alisisitiza Msama.
Msama aliomba wananchi waendelee kuipa sapoti kampuni yake kwa kuwa
imekuwa ikirejesha mapato ya viingilio na sadaka katika tamasha hilo kwa
jamii hasa kwa watu wasiojiweza, makundi maalumu pamoja na kuendeleza
vipaji vya wasanii chipukizi wa nyimbo za injili nchini kote.
Hata hivyo, wadau mbalimbali waliokuwepo katika uzinduzi huo
walisikitishwa na kutokutokea kwa mwanamuziki huyo huku wengine
wakimlalamikia kuwa na tabia hizo kwa muda mrefu na kufanya bila woga na
hofu yoyote.
Mwanamuziki huyo aliwahi kuripotiwa kutuhumiwa kufanya udanganyifu kwa
kupokea zaidi ya Sh milioni 3 na kisha kushindwa kufanya onyesho katika
tamasha la nyimbo za injili lililoandaliwa mkoani Njombe mwaka jana.
Mkurugenzi wa Kampuni ya The Comfort Gospel Promotions, Seth Sedekia,
ndiye alimfungulia kesi hiyo katika kituo kikuu cha polisi Njombe na
akapewa RB namba: NJ/RB/1793/2015.
Kushindwa kutokea kwa mwanamuziki huyo siku hiyo ya Jumapili iliyopita,
kuliwafanya mashabiki waliokuwa wamelipa kiingilio cha shilingi 5,000
kila mmoja kuzusha vurugu kubwa kwa mwandaaji huyo wakidai wametapeliwa
huku wengine wakionyesha kuchukizwa na kitendo cha mwanamuziki huyo
kushindwa kutokea kufanya onyesho hilo.
Mwandaaji wa onyesho hilo, Sedekia alisema amefikia hatua ya kufungua
kesi kituo cha polisi kufuatia kumlipa fedha zote shilingi milioni tatu
Mhando ambazo alisaini mkataba naye akiwa mjini Dodoma kwa ajili ya
kufanya onyesho mjini Njombe. Katika onyesho hilo, Mhando alitarajiwa
kushirikiana na msanii wa nyimbo za injili, Happy Kamili kutoka jijini
Mbeya ambaye alifika katika tamasha hilo akishirikiana na wasanii
wengine kutoka mjini Njombe.
Ofisa Habari wa Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Franco Malimba,
alipoulizwa juu ya kuwepo kwa taarifa hizo katika kituo cha polisi,
alikiri kuwepo lakini alisema hawezi kulizungumzia kwa sababu halijafika
ngazi za juu.
Mwimbaji Rose Mhando Ashtakiwa Kwa Waziri Nape Juu ya Utapeli Anaofanya.....
Reviewed by Mzansi
on
6:17 AM
Rating:
Reviewed by Mzansi
on
6:17 AM
Rating:
No comments: